Togo waibana Harambee Stars nyumbani

Share this

Timu ya taifa Harambee stars wamekosa nafasi ya kuchukua uongozi katika jedwali kwenye kundi G katika michuano ya kufuzu kipute cha mataifa bara Afrika almaarufu AFCON,baada ya kuandikisha sare ya 1-1 dhidi ya Togo Jumatatu usiku katika uga wa Moi sports Kasarani.
Stars walionekana kuwa na ubora zaidi na hata kutia kimiani bao katika nusu ya kwanza ya mchezo kupitia mchezaji Johana Omolo,ila bao hilo lilisawazishwa mnamo dakika ya 64 kupitia mpira wa kona ikizilazimu timu hizo mbili kwenda nyumbani na alama moja kila mmoja.
Vijana wake Francis Kimanzi waliingiwa na kiwewe baada ya mshambulizi Michael Olunga kupata jeraha katika dakika ya kumi ya mchezo ambapo alishughulikiwa na matabibu na kufanikiwa kurejea mchezoni.
Kufuatia ulizi tepetevu wa Stars,Togo walitishia kuchukua uongozi wa mechi kunako dakika ya 15 huku mchezaji Lawson akionyesha makali yake.
Nafasi ya wahedi kwa Stars ilipatikana kupitia mchezaji Johana Omollo ila mpira hukufanikiwa kutikisa nyavu na badala yake kuwazalishia kona.
Mechi hiyo ilionekana kutamatika kwa sare katika kipindi cha kwanza ila bao lake Omolo liliwaweka Stars kifua mbele kunako dakika ya 37 ya mchezo.Bingwa huyu alisukuma tofali nje ya kijisanduku na kufanikiwa kutinga bao ambalo liliwapa tabasamu mashabiki wa nyumbani ambao kwa kweli walijitokeza kiasi cha hana kuishangilia timu ya taifa.
Dakika moja baadaye vijana wa Togo walitishia kufunga bao la kusawazisha ila mlindalango Ian Otieno akamakinika zaidi na kuokoa mkwaju huo.
Stars ambao walionekana kuwa na mshawasha zaidi walifanya kila juhudi kusajili bao la pili ila muda ukawapa kisogo huku refa akipuliza kipenga kuashiria kutamatika kwa kipindi cha kwanza.
Vijana wa nyumbani walianza kipindi cha pili na uchu wa aina yake hadi pale ambapo walitishia kusajili bao la pili kunako dakika ya 47 ila juhudi zao zilikatizwa na mlinzi wa Togo ambaye ambaye alifanikiwa kuondoa mpira.Timu zote mbili zilitiana presha ila mwisho wa siku hakuna bao lililoshuhudiwa,maanake wore walionekana kuwa na nguvu sawa.
Hata hivyo baadaye kunako dakika ya 64 ,wageni Togo walifanikiwa kutia kimiani bao lao la kwanza na la kusawazisha kupitia Hakim Ouro Sama kwa kutumia kichwa .
Nahodha Victor Wanyama pia alipata nafasi ya kucheka na nyavu mnamo dakika ya 80 baada ya kupokea mpira kutoka kwa Erick Omondi ambaye alikuwa amechonga mpira wa madhambi lakini mpira ukagonga mtambaa panya na kutoka nje.
Michael Olunga pia alitulizwa maini baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa na kuzalisha mpira wa kona ambao pia hukuzalisha matunda yoyote.
Sare hii inamaanisha kwamba Stars wanasonga hadi nambari ya pili katika kundi lao nyuma ya viongozi Comoros,ambao mapema Jumatati walisajili sare tasa (0-0) na Misri.
Kwingineko Togo wanashika mkia kwenye jedwali wakiwa na alama moja pekee.

Kevin Spahlet

Read Previous

Joachim Low:Tumefuzu ila kushinda ni kitendawili

Read Next

Warning to smartphone users after man goes temporarily blind

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This content is protected.